Korea Kaskazini ilirusha makombora kadhaa ya masafa marefu baharini leo Jumatatu, jeshi la Korea Kusini limesema saa chache baada ya wanajeshi wa Korea Kusini na Marekani kuanza mazoezi yao ya pamoja ya kila mwaka ambayo Korea Kaskazini inayaona kama mazoezi ya uvamizi.
Wakuu wa majeshi ya Korea Kusini wamesema kuwa makombora hayo, tukio la tano la Korea Kaskazini la kurusha makombora mwaka huu yaligunduliwa kutoka jimbo la Hwanghae la Korea Kaskazini lakini hawakutoa maelezo zaidi kwa mfano ni umbali gani yalirushwa.
Mapema Jumatatu, wanajeshi wa Korea Kusini na Marekani walianza mazoezi yao ya pamoja ya kijeshi ya kila mwaka ambayo yamepangwa kudumu kwa siku 11. Zoezi la komandi ya Freedom Shield lilianza baada ya wanajeshi wa Korea Kusini na Marekani kusitisha mafunzo ya moja kwa moja ya ufyatuaji risasi wakati Seoul inachunguza jinsi ndege zake mbili za kivita zilivyoshambulia kimakosa eneo la raia wakati wa mazoezi ya kupasha misuli wiki iliyopita.
Kuanza kwa mazoezi hayo kulizusha shutuma za Korea Kaskazini yenye silaha za nyuklia ambayo ilitoa taarifa ya serikali ikiyaita mazoezi hayo kuwa kitendo hatari cha uchochezi ambacho kinaongeza hatari ya vita vya kijeshi.
Forum