Marekani iliweka ushuru mpya wa asilimia 25 kwenye bidhaa kutoka kwa washirika wakubwa zaidi wa biashara, Canada na Mexico wakati akiongeza maradufu ushuru wa awali wa asilimia 10 dhidi ya bidhaa kutoka China hadi asilimia 20.
Trump alichukua hatua hiyo licha ya mataifa hayo jirani kusema kwamba yalikuwa yamechukua hatua ya kudhibiti uhamiaji haramu kwenye mipaka, pamoja na uingizaji wa dawa za kulevya Marekani. Thamani kwenye soko la hisa la Marekani ilishuka kwa kiwango kikubwa muda mfupi baada ya tangazo la Trump la Jumatatu.
Trump amesema kwamba hatua hiyo huenda ikawaumiza kwa muda watumiaji wa bidhaa wa Marekani pamoja na biashara kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa kutoka mataifa yote matatu yaliyowekewa vikwazo.
Hata hivyo amesema kwamba hatimaye mataifa hayo yatalazimika kubuni viwanda ndani ya Marekani ili kuepuka kulipa ushuru wa juu. Trump aliandika kwenye mtandao wa Truth Social kwamba iwapo makampuni yatafungua viwanda vyao Marekani, kamwe hakutakuwa na ushuru.