Iran yasema haijapokea barua ya mazungumzo ya nyuklia kutoka kwa Trump

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baghaei

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema leo Jumatatu haijapokea barua kutoka kwa Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu mazungumzo ya makubaliano ya nyuklia.

Trump alisema Ijumaa kwamba alituma barua kwa uongozi wa Iran wiki iliyopita akipendekeza yafanyike mazungumzo na jamhuri ya kiislamu, ambapo mataifa ya magharibi yana hofu kwamba kwa kasi inakaribia kuwa na uwezo wa kutengeneza silaha za atomiki.

FILE - Vinu vya nyuklia vya Iran huko katika mji wa Isfahan, Iran.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Esmaeil Baghaei, amewaambia waandishi wa habari kwamba mbinu ya Marekani ya kutumia uwezekano wa kutokea vita kama njia ya mazungumzo unaonyesha kwamba hauzingatii uzito wa majadiliano na mashauriano.
Maafisa wa nchi za magharibi wana hofu kwamba Iran yenye nguvu za nyuklia, huenda ikatishia usalama wa Israel, wazalishaji mafuta wa Ghuba ya Kiarabu na kupelekea kutoka ushindani wa silaha katika kanda hiyo.
Iran imekanusha ripoti kwamba inataka kuunda silaha za nyuklia.