Ukraine yakubaliana na mpango wa Marekani wa kusitisha mapigano

  • VOA News

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio, Mshauri wa usalama wa taifa Mike Waltz, waziri wa Ukraine wa mambo ya nje Andrii Sybiha, na Mkuu wa utawala katika Ofisi ya Rais wa Ukraine, Andriy Yermak

Maafisa wa Marekani na Ukraine walikutana Jumanne mjini Jeddah, Saudi Arabia kwa mazungumzo kuhusu juhudi za kumaliza vita kati ya Russia na Ukraine, huku pande zote mbili zikisema Kyiv inaunga mkono mpango wa Marekani wa sitisho la mapigano kwa siku 30.

Taarifa ya pamoja baada ya mazungumzo imesema, “ Ukraine imeeleza iko tayari kukubali pendekezo la Marekani kutekeleza mara moja sitisho la mapigano kwa siku 30, ambalo itabidi likubaliwe na pande zote, ambalo pia lazima litekelezwe na Russia. Marekani itawasiliana na Russia kwa sababu ridha yake kwa mpango huo ni muhimu ili kufikia amani.”

Imeongeza kwamba Marekani itaondoa mara moja hatua ya kusitisha kushirikiana taarifa za kijasusi na kuanza kutoa tena misaada ya kiusalama kwa Ukraine.

Waziri wa mambo ya nje Marco Rubio na mshauri wa usalama wa taifa Mike Walz waliongoza ujumbe wa Marekani kwenye mazungumzo hayo ya Jeddah kufuatia juhudi za Rais Donald Trump kutaka vita vilivyoanza mapema mwaka 2022 baada ya Russia kuivamia Ukraine vimalizike.