Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Aprili 29, 2025 Local time: 20:18

Tanzania yasema watu wawili wamegundulika kuwa na maambukizi ya Mpox


Afisa wa serikali akichukua vipimo vya joto wakati wa uzinduzi wa kampeni ya chanjo ya mpox huko DRC October 5, 2024. Picha na AFP
Afisa wa serikali akichukua vipimo vya joto wakati wa uzinduzi wa kampeni ya chanjo ya mpox huko DRC October 5, 2024. Picha na AFP

Wizara ya Afya nchini Tanzania Jumatatu imesema kuwa watu wawili (2) wamegundulika kuwa na maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Mpox.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotelewa na Waziri wa Afya nchini humo Mhe. Jenista Mhagama imesema kuwa watu hao wamegundulika kutokana na wizara hiyo kupitia mifumo yake ya ukusanyaji taarifa na ufuataliaji wa mgonjwa iliyofanyika mnamo Machi 7, 2025 ambayo ilibaini uwepo wa wahisiwa wenye dalili za vipele usononi,mikononi,miguuni na sehemu nyingine za mwili.

Licha ya taarifa hiyo kutofafanua kwa kina wagonjwa hao walip, lakini imeongeza kwa kusema kuwa, mhisiwa mmoja wa ugonjwa huo ni dereva wa magari ya mizigo aliyetoka nchi jirani kwenda Dar es Salaam.

“Tulichukua sampuli zao na kwenda kuzipima maabara na uchunguzi imethibitishwa kuwa wahisiwa wawili wana maambukizi ya virusi vinavyosababisha Mpox,”. Alisema Waziri Mhagama kwenye taarifa yake.

Waziri Mhagama ameongeza kwa kusema kuwa, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI na vituo vyote vya kutolea huduma za Afya, inaendelea na ufuatiliaji, uchunguzi na utambuzi kubaini kama kuna wahisiwa wengine wa ugonwa huo ili waweze kupatiwa huduma stahiki za matibabu.

Hata hivyo Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya imewataka wananchi kuendelea kuzingatia na kutekeleza afua za kujikinga na ugonjwa huo kwa kunawa mikono na maji tiririka, kuepuka kuchangia vitu kwama nguo na kuwahi katika kituo cha huduma za afya kwa uchunguzi na matibabu wanapoona mojawapo ya dalili za ugonjwa huo.

Ikukumbukwe kuwa Shirika la Afya Duniani (WHO),ilitangaza ugonjwa huo kuwa wa dharura mnamo Agusti 2024 baada ya kugundulika rasmi mwaka 2022 na pia kuongezeka kwa visa katika nchi ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC) na kuenea nchi jirani ikiwemo Rwanda.


Forum

XS
SM
MD
LG