Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Aprili 29, 2025 Local time: 20:12

Wanawake Tanzania waitaka serekali kuboresha huduma za afya kwao


Rais wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, akihutubia wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake, Tanzania.
Rais wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, akihutubia wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake, Tanzania.

Tanzania imeungana na mataifa mengine ulimwenguni kusheherekea Siku ya Kimataifa ya  Wanawake, maadhimisho ya kitaifa yakifanyika mkoani Arusha. Katika maadhimisho hayo, wanawake wameitaka serikali kuendelea kuboresha huduma za afya, hasa kwa wanawake wenye umri mkubwa.

Wanawake hao wanasema kuwa hatua hiyo itawasaidia kuimarisha ustawi wao na kuepuka maradhi yanayoweza kuzuilika.

Mmoja wa wanawake hao, Julieta Temba, mkazi wa Arusha, amesisitiza umuhimu wa kuboresha huduma hizo, akisema "Tunaomba tuboreshewe kwa upande wa afya, tuwe na matibabu mazuri hasa kwa wale wenye umri mkubwa kuanzia miaka 50 kwenda juu. Tunamwomba Rais Samia atusaidie."

Kwa upande wa wanawake wa jamii za wafugaji, hali inaonekana kubadilika kwa kiasi kikubwa. Wanasema kuwa tofauti na miaka ya nyuma, sasa wanapata elimu na fursa zaidi, ikiwa ni matokeo ya ujenzi wa shule vijijini na juhudi za kuhakikisha watoto wa kike na wa kiume wanapata haki sawa ya elimu.

Lucia Balewa, mkazi wa Arusha na mmoja wa wanawake wa jamii ya Wamasai, amesema: "Kwa sasa jamii yetu inaendelea. Tunapata elimu. Mimi mwenyewe nimesomeshwa na sasa niko kijijini ninafundisha wenzangu Wamasai.”

Belwa ameongeza kuwa “Wanawake wameanza kuonekana katika kila idara kwasasa kuna wakurugenzi, walimu, wakuu wa wilaya, na hata wakuu wa mikoa ambao ni Wamasai."

Wanawake wa Kimasai walioshiriki siku ya Wanawake Duniani, jijini Arusha, Tanzania.
Wanawake wa Kimasai walioshiriki siku ya Wanawake Duniani, jijini Arusha, Tanzania.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akihutubia maadhimisho hayo, amesisitiza kuwa jamii inapaswa kujenga kizazi kinachojiamini, chenye uwezo wa kujenga hoja zenye mantiki badala ya kutumia ukali wa sauti au maneno makali.

"Tujenge vijana wanaojitambua kwamba madai ya usawa wa kijinsia ni madai halali kwa mujibu wa Ibara ya 12 ya Katiba yetu. Siyo jambo la kudhushwa na Doros Gwajima au jambo la kuzushwa na serikali. Ni madai halali kwa mujibu wa Katiba yetu," amesema Rais Samia.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa mwaka 2025, "Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa, na Uwezeshaji," inabeba ujumbe wenye uzito mkubwa kuhusu nafasi ya wanawake na wasichana katika jamii.

Forum

XS
SM
MD
LG